Maswali na Majibu

Kipi kilikuhamasisha kufanya filamu hii?

Watu na utamaduni wa Kiswahili wa pwani ndio ulizonihamasisha sana kutengeneza filamu hii. Filamu hii pia inajaribu kuwasilisha ujumbe kuhusiana na malaria wakati wa uja uzito. Malaria inaweza kutokomezwa Tanzania, kama ilivyokuwa katika maeneo mengine duniani. Ni tegemeo letu kuwa filamu hii itasaidia sana katika mapambano dhidi ya malaria.

Ni upi ujumbe mahsusi wa filamu hii?

Kuna taarifa nyingi muhimu zinazotokana na filamu hii. Hadithi nzima katika filamu hii inawahamasisha vijana kupigania kile wakitakacho katika maisha yao. Ni muhimu kutokukata tamaa katika ndoto zako. Badala yake jaribu kuzifanya ziwe za kweli. Mara nyingi ni siri zetu wenyewe ndizo huwa adui zetu wakubwa, na hisia zetu tunazozificha zinaweza kutuumiza sana. Kwenye filamu hii kuna taarifa maalumu za afya zinazohusiana na uzuiaji wa malaria wakati wa ujauzito. Ni muhimu sana kwa waja wazito kuwahi kwenda kliniki mara tu wanapobaini kuwa ni waja wazito. Huko watajifunza umuhimu wa vyandarua na dawa zitakazozuia kupata malaria wakiwa waja wazito.

Huu mradi ulikujaje?

Mradi huu uliagizwa na JHU-CCP, wakishirikiana na USAID kama sehemu ya juhudi za kuzuia Malaria. Ni imani yetu hapa MFDI kuwa elimu lazima iburudishe kwa namna moja au nyingine, na ndio maana tulianza kazi na mswada uliogusa masuala ya Malaria katika njia inayohusisha hadhira, na kuibua majadiliano yake kutokana na hiyo hadithi inayofariji mioyo.

Changamoto zipi mlizipata katika kutengeneza filamu kwenye maeneo ya vijijini Tanzania?

Filamu ilipigwa Buyuni, kijiji kilichoko mbali, katika ukanda wa pwani wa Tanzania. Ni eneo ambalo halina umeme, wala maji ya mabomba na barabara ni mbovu sana. Tuliipiga filamu mwishoni mwa msimu wa mvua, hali iliyosababisha barabara nyingi kufunikwa na maji na moja ya madaraja kuzolewa. Tunawashukuru wana kijiji waliotusaidia kulijenga tena daraja na kurahisisha kupeleka vifaa kwenye maeneo ya kupigia picha. Hata hivyo, pamoja na changamoto zote hizo Buyuni lilikuwa eneo mahsusi na halisi la hii filamu, kwani umbali wake ulisaidia kuwaweka karibu wahusika na mafundi.

Filamu hii itawavutia watu gani hasa?

Filamu hii ilitengenezewa hadhira ya Watanzania kwa ujumla. Nafikiri kila mmoja ataifurahia filamu hii, vijana kwa wazee, kutokea Dar es Salaam hadi Mwanza na kwingineko.

Filamu hii ina nafasi gani katika Tasnia ya filamu za Kiswahili?

Moja ya malengo yetu makubwa hapa MFDI ni kusaidia kujenga uwezo wa Wacheza filamu Wakulipwa wa Kitanzania. Watanzania wanapenda filamu, na tasnia yake inakua hapa Dar es Salaam inayoweza kufananishwa na mwanzo wa Filamu za Kinaijeria, ‘Nollywood.’ Hali hii inatusisimua sana, kwani ni tasnia inayokua kulingana na wakati.

Maisha ya Muongozaji

Muongozaji wa ‘Chumo’ Jordan Riber amekulia Harare, Zimbabwe, ni mtoto wa kiume wa Watengeneza filamu maarufu John na Louise Riber. Akiwa amekulia katika mazingira ya vifaa vya filamu na matayarisho yake, alipata uzowefu wake wa mwanzo kama injinia wa sauti kwenye studio za MFDI huko Harare. Miaka mitano iliyopita, Jordan alihamia Tanzania na kujishughulisha zaidi katika utayarishaji na uongozaji katika filamu na radio. Hivi sasa anaishi Dar es Salaam, mtengenezaji filamu kijana mwenye mwanga wa maisha bora ya baadaye. Kilicho muhimu kwake hivi sasa ni kukua kama mtengeneza filamu, na wakati huo huo kuchangia katika kuwakuza watengeneza filamu vijana kama yeye hapa Tanzania. ‘Chumo’ ni filamu yake ya kwanza.

Wahusika Wakuu

Juma - Hussein Mkiety Amina - Jokate Mwegelo Yustus - Yusuph Milela Ali - Jafari Makati

...Ona Zaidi